Kwanini Unajizuia Kupenda? "Bwana Ndimbo" - hamasisha

Monday, September 25, 2017

Kwanini Unajizuia Kupenda? "Bwana Ndimbo"

Hivi unaweza kujizuia kumpenda sana mtu? Wala usikatae, hapa jibu laweza kuwa ndiyo. Ila baada ya kufanikiwa kujizuia kupenda sana utakuwa umetengeneza mazingira gani katika mahusiano yako? Unadhani mahusiano yako yatakuwa na afya?
Kama ulikuwa unajidanganya kuwa unapojizuia kupenda ndiyo uta’enjoy’ mapenzi jua umekosea. Kwanini?
Ili kufanikiwa katika dhamira yako hiyo, kuna baadhi ya mambo ya kimapenzi itabidi tu uyapunguze. Yaweza kuwa mawasiliano, kiwango cha uaminifu, heshima au jinsi ya kumjali. Sasa miongoni mwa mambo hayo yanapokosekana katika uhusiano bado utasema upo katika mahusiano timilifu? Jibu unalo.
Mapenzi yana taratibu na misingi yake kama ilivyo baadhi ya vitu. Ili uwe katika mahusiano ya amani ni lazima kanuni hizo zifuatwe.
Kitu cha msingi si kuangalia jinsi ya kutopenda sana bali ni kuongeza umakini wakati wa kuanzisha mahusiano yako.
Hivi kuna binadamu kamili ambaye hapendi kuona akipendwa sana? Hapana. Sasa vipi anapoona anampenda mtu asionesha kumpenda sana? Ataendelea kuwa naye? Ili iweje?
Ukweli ni kwamba ni lazima aangalie mustakabali mwingine. Uzoefu unaoonesha kuwa watu wengi wanaodumu katika mahusiano ni wale wanaoonesha kupendana sana. Huku wale wasionesha hali hiyo wamekuwa watu wakuachana kila uchao. Hakuna mtu asiyependa kupendwa. Kila mtu anapenda kujihisi ni muhimu na wa thamani kwa mwenzake. Na njia sahihi ya kuonesha suala hili vizuri ni kupitia kiwango cha juu cha upendo utakachomuonesha mwenzako.
Hata watoto wadogo wanapenda kuona wakipendwa sana na wazazi wao. Pindi wanapoona mzazi wao mmoja hawapendi kama yule mwingine basi na wenyewe huelekeza upendo wao wote kwa yule anaonesha kuwapenda. Sasa vipi kwa mtu mzima mwenye akili timamu na mwenye kujua thamani na maana halisi ya upendo? Bila shaka jibu unalo
Kama kweli unampenda mtu kwa dhati hakutokuwa na suala la kujizuia kumpenda. Mapenzi ni kupendana, achana na hizo dhana za zisizokuwa na maana, jiachie ufurahie mapenzi.
Mtu asiye kupenda na limbukeni ndio pekee anaweza kukufanyia vitimbi baada ya kugundua unampenda na siyo zaidi ya huyo.
USHAURI: Zidisha umakini na utulivu wakati unachagua mtu wa kuwa naye. Ni sumu kukurupuka. Unapokurupuka ndipo unaweza kuona kwamba ulifanya kosa kumpenda sana fulani

No comments:

Post a Comment